Featured Post
HERI NIWE PEKE YANGU-SEHEMU YA 05
- Get link
- X
- Other Apps
Nyumbani kwa Felix paligeuka uwanja wa malumbano usiku ule. Abigail alifoka sana akitaka ifikapo kesho yake asubuhi arudi hospitalini Bugando kumjulia hali Jonathan.
Wakati huohuo Felix alimpa onyo na kumwambia asikanyage hospitalini wala kituo cha polisi labda afanye hivyo kama askari watamhitaji kufanya hivyo.
Abigail hakujali aliamua kuchukua ufunguo wa gari yake aliokuwa ameutupia kitandani kisha alitoka nje na kuwasha gari. Aliondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea Bugando pasipo kujali kama muda mfupi uliopita alikamatwa akiwa palepale hospitalini.
Alipofika katika geti la hospitali, walinzi walimzuia kuingia kwani muda wa kuwaona wagonjwa ulikuwa umefika tamati hakuruhusiwa mtu yeyote kupita getini isipokuwa wagonjwa na wenye wagonjwa tu ndiyo waliruhusiwa. Abigail alilia sana akiwaomba walinzi wa getini wamruhusu akamuone Jonathan. Ilikuwa ni bahati yake tu kukubaliwa. Aliingia moja kwa moja wodini alipokuwa amelazwa Jonathan.
Alimsogelea na kuanza kumsemesha. “Jonathan tafadhali amka useme name,” Taratibu Jonathan alifungua macho yake na kumtazama Abigail usoni. Kwa sauti ya chini sana alisema: “Abigail najua unanipenda sana lakini naomba ujikaze unisikilize. Naomba kesho uende kituo cha polisi ufungue kesi ya mashitaka ya kumshitaki mfanya biashara ajulikanae kwa jina la Mac.
Waambie maaskari kuwa yeye ndiye aliyenipigia simu na kuniambia nimfate Usagara na baada ya kufika pale niliwakuta watu wanne kama mabondia ambao bila kupoteza muda walinikamata na kunifunga kitambaa cheusi usoni kisha walianza kunipiga bila huruma.
Niliwasikia wakisema kuwa, bosi wao kawaambia wahakikishe wanauondoa uhai wangu.” Kitendo cha Jonathan kumwambia Abigail asikilize kwa makini, kilimfanya aiweke simu yake tayari kurekodi maneno yake kama ushahidi.
“Sawa Jonathan nimekuelewa kesho asubuhi nitaenda kituo cha polisi na nitaufikisha ujumbe wako. Abigail aliondoka usiku uleule na kurudi nyumbani. Alitamani sana asubuhi ifike apeleke ujumbe aliopewa na Jonathan.
Ilikuwa yapata majira ya saa kumi na moja alfajiri, Abigail alikuwa anajiandaa kwenda kituo cha polisi kupeleka ujumbe aliopewa na Jonathan mara simu yake iliita na aliyekuwa anapiga ni Mary mfanyakazi mwenzake.
“Pole sana rafiki yangu nasikia Jonathan amefariki. Nimetoka kusikiliza taarifa ya habari hapa wametangaza kuwa, “Mfanya biashara maarufu Jonathan Mayunga amefariki dunia usiku wa kuamkia leo,” aliongea Mary.
“Unasemaje Mary! Nooo! Nooo! {hapana! hapana!},” Abigail alilia sana huku akiirusha simu yake kitandani kwa nguvu na kusema, “Jonathan wangu amefariki bila ya mimi kumwambia nilichotaka kumwambia kabla sijafunga ndoaa! Jonathan wangu ameondokaa! Alitoka nje upesi na kuingia ndani ya gari lake.
Aliendesha gari kwa kasi ya ajabu kuelekea hospitalini na akiwa katika mwendo huo wa kasi, ghafla gari aina ya Harrier ilikosea njia na kugongana na gari yake uso kwa uso. Pale pale dereva wa gari hilo alifariki na Abigail alichomoka ndani ya gari yake kupitia kioo cha mbele na kudondoka pembezoni mwa barabara na huku damu nyingi zikiwa zinachuruzika kutoka kichwani mwake.
Wasamalia wema walimchukua na kumkimbiza katika hospitali ya Bugando akiwa hajielewi kabisa. Akiwa hospitalini hapo, alipewa huduma ya kwanza kisha alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi ‘ICU’.
Huko hakujitambua kabisa na uwezo wake wa kupumua ulikuwa mdogo sana. Aliwekewa mashine ya ‘Oxygen’ kwa ajili ya kumsaidia katika upumuaji. Hali yake ilikuwa mbaya sana.
Taarifa hizo za ajali zilimfikia Felix, alihisi kuchanganyikiwa. Hakutaka kupoteza muda aliahirisha safari yake ya kwenda kazini na kuamua kuelekea hospitalini.
Mapigo yake ya moyo yakiwa mbio sana, alijikuta akisukuma kila mtu aliyekuwa mbele yake ili apate upenyo wa kupita kuelekea chumba cha wagonjwa mahututi alipokuwa amelazwa mchumba wake Abigail.
Hakuamini kile alichokiona baada ya kumuona mpenzi wake akiwa amefungwa bandeji kichwa kizima na mwili wake ukiwa na mirija kila mahali.
Alijikuta akipiga kelele za kilio kwa nguvu na kupelekea madaktari kumuondoa katika chumba hicho. “Daktari, daktari, niambieni ukweli kama mpenzi wangu bado yupo hai. Niambieni tafadhari!” Felix alilia kwa uchungu.
Baada ya siku mbili utaratibu wa mazishi ya Jonathan ulifanyika na hatimaye alipumzishwa katika nyumba yake ya milele pasipo Abigail kushuhudia safari yake ya mwisho.
Ndugu wa marehemu walichukua jukumu la kusimamia mali zake na biashara yake. Kwa kuwa Magreth hakuwa anatambulika katika familia yake, basi hakuambulia kitu chochote na hivyo kupelekea majonzi makubwa sana kwake.
Baada ya Abigail kufanyiwa vipimo iligundulika kuwa amepoteza uwezo wake wa kukumbuka. Ajali iliathiri ubongo wake kwa kiasi kikubwa na kupelekea kupata tatizo hilo la kupoteza kumbu kumbu.
Hali hii ilimpelekea kukaa hospitalini kwa muda mrefu sana akiendelea kupatiwa matibabu. Kutokana na hali hiyo, uongozi wa ofisi yake ulimsimamisha kazi na kuahidi kumrejesha endapo atapona kabisa. Familia yake iliamua kuchukua jukumu la kumuhudumia.
Wazazi wake walimchukua na kumpeleka nyumbani ambapo angepata huduma kwa ukaribu zaidi. Kwa kuwa Felix alikuwa anatambulika kwao, nae alishirikiana nao bega kwa bega.
Hakika kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa Felix kwa kumpoteza aliyekuwa mfanya biashara mwenzake na wakati huo huo mke wake mtarajiwa kupata ajali mbaya iliyompatia ulemavu.
Abigail alirudi kuwa mtoto licha ya majeraha mwilini mwake kupona kabisa. Hakuweza kunena neno lolote zaidi ya kucheka tu na kujaribu kuongea baadhi ya maneno ambayo hayakueleweka kama mtoto mdogo anayejifunza kuongea.
Siku moja jioni mtoto wa Abigail alikuwa chumbani na mama yake akichezea nywele za mama yake. Katika kupepesa macho yake huku na kule, alijikuta akitizama chini ya uvungu wa kitanda. Aliona kitu kama simu ndogo hivi. Aliacha kuchezea nywele na kuinama chini ya uvungu kuichukua.
“Mama ona! nimeokota simu ndogo mama!” Aliongea Elizabeth. Abigail alicheka tu wala hakujibu lolote. Elizabeth aliichukua simu ile ndogo na kuirusha juu ya kabati la nguo lililokuwa pale chumbani kisha aliendelea kuchezea nywele za mama yake.
Hali ya kwenda nyumbani kwao Abigail kila siku kumjulia hali, ilimchosha Felix. Siku moja alipokuwa anatoka kazini akiwa ndani ya gari lake kuelekea kwao Abigail alijisemea, “Leo nakwenda kuwaambia wazazi wake kuwa mimi nipo tayari kufunga nae ndoa akiwa ndani ya hali hiyo.
Mimi nimechoka bwana! Kila siku kwenda na kurudi. Ni bora nimuoe awe nyumbani kwangu na nimuajiri mfanyakazi kwa ajili ya kumuhudumia. Nipo tayari kutoa pesa yoyote lakini sio huu usumbufu aisee!” Felix aliendelea kutafakari huo mpango wake mpaka alijikuta amefika kwao Abigail.
Alipoitazama mishale ya saa yake, tayari ilikuwa imewadia saa mbili usiku.
Usiku huo ulikuwa mzuri sana kwa familia yake Abigail kwani ilikuwa ni siku ambayo Abigail alizaliwa na muda ule ule ambao ndiyo muda aliozaliwa Abigail, wazazi wake walishangazwa kumsikia akizifungua lipsi za midomo yake na kutamka neno ‘mama’.
Hakika walifurahi sana na kwao wakaitafsiri kama hatua nzuri ya maendeleo ya kiafya ya mwanao. Hapo hapo wakiendelea kumpigia makofi Abigail huku na yeye akitabasamu kwa mbali, Felix aliongea.
“Wazazi wangu wapendwa mimi nina wazo naombeni nifunge ndoa na mke wangu mtarajiwa mwanenu. Muda wetu tulioupanga wa kufunga ndoa unakaribia bado mwezi mmoja tu tarehe ya kufunga ndoa itimie.
Nampenda sana Abigail na nipo tayari kuishi nae kwa hali yoyote ile. Niruhusuni nikamilishe mipango yote ya harusi yetu kama nilivyowaahidi hapo mwanzo kisha tualike watu wachache tu na tufunge ndoa yetu,” aliongea Felix katika hali ya kuwabembeleza wazazi wake Abigail.
Kauli ya Felix iliwashitua sana wazazi wake Abigail. Wakati baba yake akiendelea kuitafakari, mama yake alijibu. “Ni wazo zuri mwanetu nadhani tupatie mda kidogo kama wa siku tatu hivi tulijadili hili mimi na baba yako.”
******************ITAENDELEA*********************
Comments