Featured Post
Amekutumia Halafu Anakuacha? Usiumie, Fanya Haya!
- Get link
- X
- Other Apps
Amekutumia Halafu Anakuacha? Usiumie, Fanya Haya!
MUNGU ni mwema sana. Tunakutana alhamisi nyingine katika eneo letu la kuweza kupeana darasa la masuala ya uhusiano. Tunajifunza, tunatafakari kwa pamoja kuhusu maisha yetu.
Hakuna aliye mkamilifu, kila mtu anajifunza kila siku. Unaweza kujiona unajua mambo lakini kumbe kuna mwenzako anajua zaidi. Uungwana ni kujenga desturi ya kujifunza. Suala la msingi ni kuiruhusu akili yako iweze kupata vitu vipya kila siku, hakika utakuwa mtu mzuri katika familia na hata uhusiano wako wa mapenzi.
Kwa kawaida, wanadamu huwa hatupendi mambo mabaya yatutokee ila yakitokea kwa wenzetu tunayachukulia kawaida. Unamfanyia mwenzako jambo baya ukiamini kwamba wewe ni mjanja, ukiamini kwamba kwa kufanya hivyo utakuwa umemkomoa mwenzako kitu ambacho si sahihi.
Ni vyema kutambua, jambo baya ambalo hupendi wewe kufanyiwa, basi ni vyema pia usimfanyie mwenzako. Nasema hivyo kwa sababu, kwenye uhusiano watu wengi wamekuwa wakilia kutokana na mambo mabaya wanayofanyiwa na wenzi wao.
Utakuta mtu analia, alikuwa na mpenzi wake lakini ghafla tu anaanza kubadilika. Anaanza kumuonesha jeuri au hata kumuoneshea mpenzi mwingine. Unakuta mtu amehangaika na mwenzake kwa muda mrefu, wametoka mbali lakini ghafla tu mambo yanabadilika.
Mlipanga kufanya naye maisha. Mlijiandaa katika kufanya mambo mengi makubwa ya maisha yenu, mathalan mlitaka kuchumbiana na hata baadaye kuoana, ghafla mwenzako anaingia mitini kabla hamjafanikisha malengo yenu.
Inauma. Inahuzunisha sababu ahadi zenu zinayeyuka katika kipindi ambacho hukutegemea. Ni kipindi ambacho akili na mawazo yako yote uliyatupa kwa mwenzako na mwisho wa siku anakuangusha kirahisi tu. Akili yako inateseka kwa mawazo.
Unaumia kwa sababu unampenda. Hauhitaji kumuona amekwenda mbali na wewe. Bahati mbaya sana, binadamu anapokuwa amempenda mtu, wakati mwingine hujikuta ameingiwa na kama upofu ndani yake. Anashindwa kung’amua mambo pengine mwenzake hakumpenda tangu mwanzo.
Yawezekana alikuwa anajifanya anampenda kumbe hampendi. Anaye mtu anayempenda. Yeye anamfanya kama daraja la safari yake ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio. Unabaki unalia peke yako baada ya kukukimbia.
NINI CHA KUFANYA?
Unapokutana na changamoto kama hii, japo inaumiza lakini ifike mahali uamue kupiga moyo konde. Sema inatosha kwa wewe kuwa na maumivu, ifike mahali na wewe ukatae mateso ili kuweza kuishi kwa raha kama binadamu wengine.
Mlipanga mengi ndio, mlikuwa na mikakati mingi sana ya maisha, ilikuwa mchumbiane na hadi kuoana lakini imeshindikana. Uliweka nguvu nyingi, akili na hata fedha kumsaidia mwenzako pale mlipokuwa pamoja, inakuuma? Wewe samehe!
Mshukuru Mungu na kile ulichokitoa, kichukulie kama umetoa sadaka kwa watoto yatima au kwa mtu yeyote aliyekuwa na uhitaji.
Amua kuamka na kupambana upya. Suala la yeye kukupotezea muda lisikuumize kichwa, muache ashughulikiwe na Mungu wake, wewe shughulikia furaha yako kwani ndio kila kitu.
Itafute amani ya moyo kwa gharama yoyote. Fedha, mpenzi mwingine vyote vitakuja tu. Mungu amekupa uwezo wa kutafuta, Mungu anaweza kukupa sawa sawa na hitaji lako.
Utampata mtu ambaye ni sahihi. Utasahau mapito yote, niamini mimi Mungu kamwe hatakuacha uteseke!
Comments