Featured Post
Chimbuko la Illuminati na dhana kuhusu nguvu zao
- Get link
- X
- Other Apps
Chimbuko la Illuminati na dhana kuhusu nguvu zao
Ni simulizi ya ulaji njama ambayo bila shaka imevuma zaidi kushinda njama nyingine zote. Ni wachache sana ambao hawajawahi kusikia kuwahusu Illuminati.
Huaminika kuwa kundi maalum la watu ambao hudhibiti masuala na uongozi wa dunia, na inasadikika kuwa hufanya shughuli zao kisiri kudhibiti kila kitu na kuunda Utawala Mpya wa Dunia.
Kwa wengine, wamehusishwa na utajiri wa ghafla ambao si wa kawaida.
Ukitajirika haraka, kunao bila shaka watakaodai kwamba umejiunga na Illuminati.
Je, kuna ukweli wowote kuhusu wasiwasi huu? Kuna kundi la watu wanaofanya vikao vya siri kupanga njama za kuitawala dunia na pia kjifaidi wenyewe kwa pesa na utajiri?
Simulizi hizi na umaarufu wa illuminati zina ukweli wowote?
Wasiwasi huu kuhusu kundi linalopanga njama ya kuweka utawala mpya duniani ulianza miaka ya 1960, sana kutokana na ubunifu wa watu fulani.
Kuenea kwa habari hizo kunatoa viashiria fulani kuhusu jinsi binadamu walivyo tayari kuamini mambo wanayoyasikia au kuyasoma, kwa urahisi sana. Aidha, kunaweza kutoa funzo kuu kuhusu taarifa na habari za uongo ambazo zinaenezwa mtandaoni siku hizi.
Kwa kuchunguza kuhusu historia ya illuminati, kwa kuanzia huwa ni nchini Ujerumani, Enzi za Kuelimika au Kustaarabika barani Ulaya (1685-1815) ambapo kulikuwa na kundi lililofahamika kama Kundi la Illuminati.
Lilikuwa ni kundi la usiri sana ambalo lilianzishwa mwaka 1776 katika eneo la Bavaria.
Wanachama wake walikuwa watu walioelimika na wasomi na kusudi lao lilikuwa kuungana na kupinga pamoja na kukabiliana na ushawishi wa makundi ya kidini na wasomi wengine katika maisha ya kawaida ya kila siku.
Kundi hilo liliwajumuisha watu kadha maarufu waliokuwa wasomi au wapenda maendeleo wakati huo. Kulikuwa pia na wanachama wa Freemason (wamasoni).
Walijipata wakipingwa vikali na makundi ya wahafidhina na Wakristo na mwishowe kupigwa marufuku. Ushawishi wao ulififia na hawakusikika tena kwa muda mrefu.
Ilikuwa ni hadi miaka ya 1960 ambapo walianza kutajwa tena.
Illuminati tunaowasikia sasa hawajakuwa na uhusiano mwingi na Illuminati waliokuwepo Bavaria enzi hizo, kama anavyosimulia mwandishi na mtangazaji David Bramwell, mwanamume ambaye ameangazia maisha yake katika kunakili na kutoa ufafanuzi kuhusu asili ya hadithi na imani nyingi za kushangaza.
Kitabu cha utani wa kidini
Badala ya kuwa na uhusiano na watu hao wa Bavaria, desturi ya kupinga utamaduni uliokubalika, kutumiwa kwa kemikali ya LSD (lysergic acid diethylamide) iliyoweza kubadili hisia za mtu pamoja na watu kutaka kujua sana kuhusu falsafa ya jamii za Asia na Mashariki ya Mbali kulichangia sana kuvuma tena kwa kundi hilo.
Hili lilianzia ulimwengu ukiendelea kushangazwa na kuvuma kwa utamaduni na mitindo mipya ya hippie pale kitabu kidogo kwa jina Principia Discordia kilipoanza kusambazwa.
Kilikuwa kitabu cha utani wa kidini, kuhusu dini ya utani ambayo ilipewa jina Discordianism.
Kitabu hicho kiliandikwa na Greg Hill na Kerry Wendell Thornley mwaka 1963, wakitumia lakabu Malaclypse the Younger na Omar Khayyam Ravenhurst
Waliwataka wasomaji kuvutiwa na kuanza kuabudu miungu kwa jina Eris au Disordia, miungu wa kike wa vurugu.
Vuguvugu hilo la Discordianism na wafuasi wake walitamani kuwe na kutotii sheria, utani mwingi na visa vingi vya watu kuhadaiwa
Kitabu hicho kimsingi kilikuwa cha kupinga utamaduni, lakini waliokiendeleza walikuwa na imani kwamba kinaweza kusababisha mabadiliko katika mtazamo wa jamii na kuibua maswali kuhusu uhalisia, kama alivyokuwa anaamini mwandishi mwingine Robert Anton Wilson.
Mwingine David Bramwell anaamini kwamba ilikuwa ni njia ya kuwazindua watu kutambua uhalisia tofauti.
Kwa mujibu wa Bramwell, Wilson na mmoja wa waandishi wa Principia Discordia, Kerry Thornley, "waliamua kwamba ulimwengu ulikuwa unageuka kuwa wa kiimla sana, wenye kudhibitiwa sana, kuwa na mipanga mingi na kutawaliwa sana".
Walitaka kurejesha vurugu tena kwenye jamii na kutikisa mambo.
Na "njia pekee ilikuwa kueneza habari za kupotosha. Kueneza habari za kupotosha kupitia majukwaa yote - kupitia utamaduni wa kupinga utamaduni uliokubalika katika jamii, kupitia vyombo vikuu vya habari na kupitia njia nyingine zozote zile. Na waliamua kwamba wangelifanya hilo mwanzoni kwa kuwaambia watu kuhusu Illuminati."
Wakati huo Wilson alikuwa anafanya kazi katika jarida lililokuwa linachapisha picha za utupu la Playboy.
Yeye na Thornley walianza kutuma barua bandia kutoka kwa wasomaji wakizungumzia shirika hilo la usiri mkubwa linaloendeshwa na wasomi na watu wenye uwezo ambalo walisema linaitwa Illuminati. Walikuwa hata wanatuma barua nyingine tofauti za kupinga barua ambazo walikuwa wametuma awali.
"Hivyo basi, dhana waliyokuwa nayo ni kwamba ukitoa mambo mengi na ya kutosha ya kupinga jambo, kinadharia - kimsingi - watu wengi wataanza kutazama na kuchungumza ammbo hayo na kufikiria, 'hebu kidogo'," anasema Bramwell. "Wanajiuliza, 'Je, ninaweza kuamini habari hizi ambazo nimepewa?' Ni njia rahisi ya kuwazindua watu na kuwafanya wafikirie kuhusu uhalisia mwingine wanaopendekezewa na watu wengine kuhusu dunia wanayoishi - jambo ambalo halikufanyika walivyokuwa wanatumai lingefanyika."
Vurugu za uvumi huu kuhusu kuwepo kwa Illuminati zilienea sana.
Wilson na mwandishi mwingine wa Playboy waliandika The Illuminatus! - msururu wa vitabu vitatu ambapo walidai kwamba Illuminati walihusika katika 'kuficha' siri kubwa ikiwa ni pamoja na kwa mfano nani aliyemuua John F Kennedy.
Kitabu hicho kilipata umaarufu sana kiasi kwamba kilifanywa mchezo wa kuigiza Liverpool, na kikawasaidia waigizaji Waingereza Bill Nighy na Jim Broadbent kupata umaarufu mwingi pia.
Leo hii, dhana ya kuwepo kwa Illuminati ni miongoni mwa njama za kudhaniwa ambazo zimefanyiwa utani zaidi duniani.
Bendi ya Uingereza ya The KLF wenyewe walijiita The Justified Ancients of Mu Mu, wakichukua jina la bendi ya watu wa Discordian ambao wanafanikiwa kuingia kisiri ndani ya kundi la Illuminati bila yao kutambuliwa na wanachama wa kundi hilo katika msururu wa vitabu hivyo vitatu vyake Wilson. Bendi hiyo ilikuwa imehamasishwa na falsafa ya vurugu ambayo ilikuwa imeendelezwa kwenye dini hiyo ya utani.
Mwaka 1975, kulitokea mchezo wa Kamari wa kadi ambapo wahusika walikuwa wanaigiza wahusika wa Illuminati. Hilo lilisaidia kuvumisha zaidi habari za kuwepo kwa kundi kama hilo.
Aidha, mchezo huo ulisaidia kuingiza dhana hiyo ya Illuminati kwa kizazi kingine.
Siku hizi, ni moja ya njama ambazo zimefanyiwa utani zaidi na zisizoeleweka.
Wasanii mashuhuri duniani kama vile Jay-Z na Beyoncé walikumbatia ishara za kundi hilo dhahania wenyewe. Wameonekana mara nyingi wakiinua mikono yao na kuunda umbo la pembe tatu wakiwa kwenye tamasha.
Haya yote hayajasababisha ufunuo - kwamba si kundi la uhalisia - kama walivyokusudia waasisi wa dini hiyo ya utani ya Discordianism.
Hali sasa ni tofauti sana na zamani ambapo mfano miaka ya 1960 wazo hili lilipoimbuliwa wachapishaji walikuwa wadogo na vitabu havikuweza kuenezwa sana. Hilo lilipunguza kuenea kwa mawazo mbalimbali, yakiwemo ya uwepo wa Illuminati.
Sasa hivi kuna utandawazi na mtandao, na habari huenea kwa haraka. Hapana shaka kwamba mtandao wa Intaneti ndio uliochangia zaidi kueneza uvumi na dhana kuhusu Illuminati, katika mitandao ya kijamii kama vile 4chan na Reddit. Hili limechangia kupata umaarufu kwa dhana hii ya Illuminati.
Huwa tunaishi katika ulimwengu uliojaa nadharia za uongo, njama na taarifa za vigwena na zaidi kunao wanaoamini mambo haya yote kuwa ya kweli.
Mwaka 2015, watafiti wa sayansi ya siasa waligundua kwamba karibu nusu ya wananchi nchini Marekani huamini angalu dhana moja ya uongo kuwa ni ya kweli.
Wanaamini mambo mengi sana kuanzia kuwepo kwa Illuminati hadi kwamba Obama alizaliwa Kenya. Wengine wanaamini kwamba mashirika ya kijasusi ya Marekani yenyewe ndiyo yaliyotekeleza shambulio la 9/11 katika jumba la World Trade Centre.
"Hakuna sifa maalum ambazo unaweza kusema watu wanaoamini mambo haya huwa nazo," anasema Viren Swami, profesa wa saikolojia ya jamii katika chuo kikuu cha Anglia.
"Kuna mitazamo mingi kuhusu ni kwa nini watu huamini dhana hizi, ambayo haifanani. Ufafanuzi wa kawaida huwa kwamba wanaoamini njama na dhana hizi kwamba ni za kweli huwa wana tatizo fulani la kisaikolojia."
Kitu kingine ambacho watafiti wameeleza kwamba huenda kikachangia kuaminika kwa dhana hizi ni kwamba nyingi huonekana kutoa ufafanuzi wa kueleweka kuhusu mambo ambayo yamekuwa hayaeleweki kamwe au yanayotishia Imani na kujiamini kwa mtu mwenyewe.
"Huwa zinakupa ufafanuzi rahisi sana (kuuelewa)," anasema Swami, ambaye alichapisha matokeo ya utafiti wake 2016.
Kwenye utafiti huo wake, aligundua kwamba walioamini njama hizo na dhana hizo kwamba ni za kweli walikuwa na uwezekano wa juu sana kwamba wanatatizwa na msongo wa mawazo au walikumbana na jambo la kuwashtua sana wakati mmoja maishani ukilinganisha na wale ambao hawaamini kuna njama kama hizo.
Watafiti wengine wamegundua kwamba watu wenye viwango vya juu vya elimu wana uwezekano mdogo sana wa kuamini dhana na njama hizo.
Jambo ambalo sasa ni tofauti na lina athari kubwa ni kwamba wanasiasa, kwa mfano Donald Trump, wameanza kutumia dhana hizi kujitafutia uungwaji mkono, anasema Viren Swami, wa chuo kikuu cha Anglia Ruskin
Taswira inayojitokeza kutokana na hili ni kwamba Marekani ingawa ipo kwenye enzi ya kisasa, ni taifa ambalo bado kwa kiasi kikubwa limo kwenye giza.
Hasa Swami anaamini hili akisema kumekuwa na mabadiliko katika wale ambao wamekuwa wakieneza dhana hizi.
"Asia Kusini, dhana hizi zimekuwa zikitumiwa na serikali kama njia ya kuwadhibiti raia. Lakini nchi za Magharibi, ni tofauti kabisa. Zimekuwa zikitumiwa na watu ambao hawana uwakilishi, wanajihisi hawana uwezo.
Ni kukosa uwezo kwao ambako kunachangia kuchipuka kwa dhana hizi kujaribu kuitishia au kutoa changamoto kwa serikali
Mfano kuhusu 9/11. Watu wanapokosa uwezo au kujihisi kukosa nguvu, dhana kama hizi zinaweza kupanda mbegu na kuchangia maasi na maandamano ya wananchi na hivyo kuwawezesha watu wa kawaida kuiuliza serikali maswali.
Trump na imani yake
Rais wa 45 wa Marekani Donald Trump alikuwa mmoja wa watu walioamini wazo la kundi kwa jina "birther". Alizungumza mara kwa mara kwenye vyombo vya habari kuhusu jinsi Rais Obama hakuzaliwa Hawaii na badala yake alizaliwa Kenya hivyo hakufaa kuiongoza Marekani.
Kadhalika, aliyatuhumu majimbo kadha ya Marekani kwa kutekeleza udanganyifu na ulaghai wakati wa uchaguzi wa mwaka 2016. Maafisa wake wa kampeni walilaumiwa kwa kueneza taarifa kama vile za kashfa ya Pizzagate na mauaji ya haliki ya Bowling Green, mambo ambayo hayakuwa ya kweli.
Je, Swami anaamini kwamba mabadiliko haya yataathiri siasa katika kipindi kirefu?
"Watu wanaweza kujitenga na siasa kuu za taifa na kukosa kushiriki katika michakato mingi ya kisasa iwapo wataamini njama na dhana hizi," anasema Swami.
"Wanaweza Zaidi kujihusisha na siasa za pembeni. Wanaweza kujihusisha Zaidi na mitazamo ya ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na misimamo mingine mikali."
Wazo la kuwepo kwa kundi lenye ushawishi mkubwa la kisiri - kama vile Illuminati - linaendana vyema sana kabisa na watu ambao wanajihisi kutengwa. Kwamba hawana usemi tena katika yanayoendelea.
Trump alisema alitaka kuwawakilisha na kuwa sauti ya watu kama hao, waliojihisi kutengwa, hasa katika maeneo ambayo zaidi yalikuwa ya viwanda na yalifana zaidi kiuchumi zaidi miaka ya nyuma lakini uchumi wa maeneo yao uliporomoka.
Lakini inaonekana kwamba badala yao kujihisi vyema kwamba sasa wanawakilishwa na mtu ambaye si mwanasiasa - badala ya wanasiasa ambao walikuwa wamepoteza imani nao - inaonekana kwamba watu zaidi na zaidi Marekani wana uwezekano wa juu zaidi wa kuamini hadithi kama za Illuminati zaidi kuliko awali.
"Wilson angelikuwa hai leo, angejawa na furaha, na pia kushangazwa kwa kiasi fulani," anasema David Bramwell. "Waliamini kwamba utamaduni ulikuwa umewabana watu zaidi miaka ya 1960. Lakini sasa, hisia ni kwamba watu wako huru lakini zaidi kupita kiasi. Hawadhibitiki tena.
"Labda uthabiti zaidi utatokea watu wakikabiliana na 'habari za uzushi' na propaganda. Tunaanza kufahamu jinsi mitandao ya kijamii inavyotupa mawazo na falsafa ambazo wenyewe tunataka kuziamini. Inaakisi mitazamo yetu kama chumba kikubwa cha mwangwi."
Hili likifanyika, katika mitandao ya kijamii, kwa walio na usemi katika utamaduni na jamii, na kwa kutumia uwezo wa binadamu wa kufikiria, basi itakuwa rahisi kwa watetezi wa ukweli kupuuzilia mbali dhana kama vile ya kuwepo kwa Illuminati, daima.
Comments