Featured Post
Mjali Mwenza Wako, Naye Atakujali!
- Get link
- X
- Other Apps
Mjali Mwenza Wako, Naye Atakujali!
RAFIKI yangu, katika kipindi hiki ambacho kuna sintofahamu nyingi, kutiliana shaka na hata kutengana, ni muhimu kujenga hulka ya kujaliana pia.Iwapo umewahi kupenda au unapendana na mchumba, mpenzi au mume wako na mko katika uhusiano wa kimapenzi, jambo kubwa linaloweza kuwaunganisha ni kujaliana.
Unapopenda kwa dhati, tegemeo kubwa ni kwamba, mwenzako pia akupende kwa vitendo na siyo maneno matupu. Je, ni wangapi wamefanikiwa kuwafanya wenzao wawapende zaidi namna wanavyotaka wao?
Kati ya wengi walio katika uhusiano, ni wachache sana wamefanikiwa kufaulu mtihani huu. Wengi wao wanalalamika kuwa, wenzao hawawapendi kwa kiwango wanachotamani kupendwa.
Ni vyema ikatambulika kuwa, japokuwa mapenzi huchukuliwa kama jambo la kawaida, lakini kumpenda mtu mwingine kwa dhati, huhitaji mbinu na mikakati.Ukweli ni kwamba, hakuna mwanamke au mwanaume anayeweza kumpenda mtu kisirani, mlalamishi na asiyependa maelewano.
Hata kama mhusika alimuona mwenzake na kumpenda, kama atakuwa na tabia tata na hataki kubadilika, upendo wa mhusika utashuka na kama itawezekana, anaweza kuanzisha uhusiano na mtu mwingine.
Ni nani atampenda mwanaume mvivu, asiyejituma na mwenye kupenda zaidi starehe na watu wengine, huku akimsahau mwenzi wake? Hata kama mwanaume husika anampenda sana mwanamke huyu, ila kama matendo haya ya ovyo hayatokoma, basi mwanaume huyu anaweza kuangalia ustaarabu sehemu nyingine.Kuna mbinu za kumfanya mwandani wako azidi kukupenda na kukujali.
Azidi kukuona wa thamani na wa maana katika maisha yako.Baadhi ya akina dada hudhani urembo pekee unatosha kuwafanya wapenzi wao wazidi kuwapenda na kuwajali. Lakini uzuri wa mwanamke siyo sura pekee. Mwenendo na vitendo, ndivyo huangaliwa kwa kiasi kikubwa.
Hakuna mwanaume ambaye atafurahia kuwa na mwanamke kiburi na asiyeonesha kumjali wala kumthamini. Ni kiu ya kila mwanaume kuwa mfalme kwa mke wake. Yaani awe na kauli juu yake, awe na uwezo wa kutoa maelekezo na yakatekelezwa, awe na mwanamke mwenye kumtendea vile anavyotaka yeye.
Ni maajabu pekee ndiyo yanaweza kunusuru penzi ambalo mwanamke anajiona kidume na mbabe dhidi ya mume wake.Kwa upande wa pili, mwanamke anahitaji kuwa na mwanaume ambaye atamfanya ajiamini na ajithamini. Siyo mwanaume ambaye kila wakati ni kulalamika tu.
Badala ya kutoa dukuduku lako, unakuwa ni mlalamikaji wa mfululizo. Badala ya kupambana na changamoto za maisha, kila wakati unakuwa na visingizio visivyoeleweka.Mwanamke anataka kuwa na mtu ambaye atamfanya kuona changamoto zote wanazopitia, ni kitu cha mpito.
Unapokaa naye na kuanza kulalamika kuhusu hali ngumu, badala ya kupambana bila kelele, unaweza ukamtisha na kumtia hofu ya furaha ya maisha yake, akiwa nawe.Mwanamke anahitaji kutulia akili, si kujazwa msongo wa mawazo.
Hata kama familia mnapitia kipindi kigumu cha uchumi, si jukumu lako mwanaume kila muda kukaa na kulalamikia hali hiyo. Pambana na hali yako, hata pindi mwanamke wako akianza kulalamikia hali ngumu, ni jukumu lako kumtia nguvu tena kwa sauti ya kujiamini.
Mwanamke anataka mwanaume wa aina hii, si mwanaume ambaye kila muda anasema; “Unajua mpenzi hali hii ni ngumu sana, sijui huko mbele itakuwaje?”
Kisaikolojia ukiwa mtu wa hivi, mwanamke wako ataanza kufikiri tofauti. Mwanamke siyo mvumilivu sana wa mikikimikiki.
Hao unawaona wako kwenye mikikimikiki, wako kwenye hali hiyo kwa sababu ya mazingira magumu tu.Ili kudumisha amani na furaha katika uhusiano wako, mwanamke jitolee kwa kiwango kikubwa kwa mume wako ili naye ajione yuko na mtu sahihi kwenye maisha yake. Furaha na amani itawale kwa wote.Kwa leo naishia hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua.
Comments