Featured Post
KIFO MKONONI MWANGU-SEHEMU YA 04
- Get link
- X
- Other Apps
Mimi na polisi wenzangu tukatazamana kwa mshangao.
“Mauaji yameanza tena kwenye jiji letu!” Nikajidai kuwaambia wenzangu.
“Mauaji yalikuwa yamekoma kwa muda mrefu kutokana na kuimarisha doria zetu za usiku,” polisi mmoja akasema.
“Lakini huyu aliyearifiwa ameuawa nyumbani,” polisi mwingine akasema kisha akamtazama yule aliyetupa taarifa.
“Huyu si ameuawa nyumbani kwake?” Akamuuliza.
SASA ENDELEA…
“TAARIFA imesema ameuawa nyumbani kwake. Nafikiri anaishi pake yake.”
Kwa bahati njema nikawa kiongozi wa msafara uliopangwa kwenda huko Kwaminchi nyumbani kwa msichana huyo aliyeuawa.
Tulipofika katika mtaa huo tulikwenda nyumbani kwa mwenyekiti wa mtaa huo, akatufahamisha nyumba iliyotokea tukio hilo ingawa mimi nilikuwa ninaifahamu.
Tulipofika tulimkuta yule mjumbe aliyetupigia simu. Mjumbe mwenyewe alikuwa mwanamke. Mbali ya yeye, tulikuta watu kadhaa wakiwa wameizunguka nyumba hiyo. Si unajua panapotokea tatizo watu hujazana kutaka kujua kumetokea nini?
Tuliingia ndani ya nyumba hiyo na kuikuta ile maiti mahali palepale nilipoiacha.
“Kumetokea nini?” Nikajidai kumuuliza yule mjumbe.
“Kilichotokea hatukifahamu. Huyu msichana ambaye ni jirani yetu na ni mwenzetu amekutwa ameuawa hii asubuhi.”
“Mtu wa kwanza kugundua kuwa kuna maiti humu ndani ni nani?”
Mwanamke huyo alinywea kabla ya kujibu.
“Ni mimi.”
“Mbona umenywea?”
“Hapana, sijanywea. Tunazungumza.”
“Uliigunduaje hii maiti?”
“Nilikuwa nimekuja kufuata mchango wa maziko. Katika mtaa wetu tuna chama chetu cha kuzikana. Mtu anapokufa watu wengine wanatoa mchango wa gharama ya maziko au kusafirisha maiti kama inapelekwa mji mwingine. Sasa nilikuja kufuata mchango wake. Kuna mtu alifariki dunia jana katika mtaa wetu na maiti yake bado iko Hospitali ya Bombo.”
Mwanamke huyo akaendelea kutueleza.
“Sasa nilipofika nikakuta mlango umesindikwa, nikabisha hodi kwa muda mrefu, lakini sikupata jibu. Nilipousukuma mlango ndiyo nikaiona hiyo maiti.”
“Baada ya kuiona ulichukua hatua gani?”
“Nilkwenda kumuarifu mwenyekiti wangu kisha nikapiga simu polisi.”
Uchunguzi wa kwanza tuliofanya mimi na polisi mwenzangu ni kuchunguza mlango wa mbele ili kujua kama ulikuwa umevunjwa au ulifunguliwa kabla ya msichana huyo kuuawa. Tuligundua kuwa mlango haukuvunjwa bali msichana mwenyewe ndiye aliyeufungua.
Tukachunguza pia kama kulikuwa na kitu kilichoibwa. Pia tuligundua kuwa hakukuwa na kitu kilichoibwa. Kulikuwa na vitu vingi vya thamani vinavyobebeka kirahisi ambavyo vilikuwepo. Kama kungefanyika wizi wowote, vitu hivyo pia visingekuwepo.
Kwa kule kuviona vitu hivyo sebuleni na chumbani kwa msichana huyo tuligundua hakukuwa na kitu kilichoibwa.
Hapo tuligundua kuwa mtu aliyemuua aliingia humo ndani kwa ajili ya kufanya mauaji hayo kisha akaondoka.
Kwa kawaida polisi tunajaribu kukisia kila kitu tunapokuwa katika uchunguzi wetu. Tulihisi kwamba mtu huyo alifika usiku na kubisha mlango. Msichana alipomfungulia ndipo alimpiga na kitu kizito, akamuua na kuondoka.
“Lakini mimi naona si rahisi kwa mwanamke kumfungulia mlango mtu asiyemjua wakati wa usiku.” Polisi mmoja akatoa hoja yake.
“Wewe ndiye unasema kwamba mtu asiyemfahamu na mimi nakubaliana na hoja yako. Kwa vile tumeridhika kwamba ni msichana mwenyewe aliyemfungulia mlango, basi tuchukulie kwamba alikuwa mtu anayemfahamu. Pengine alimuuliza nani wewe, akajitambulisha ni nani.” Nikamwambia polisi huyo.
“Okey, inawezekana ni mtu anayemfamu.”
“Kama ni hivyo tutafute alimuua kwa kitu gani kisha tutafute mtu huyo anaweza kuwa ni nani.” Nikaendelea kutoa muongozo.
“Sawa afande,” polisi mmoja akanikubalia.
“Hapa kuna vipande vya chupa ya bia vyenye damu. Inaonesha kwamba msichana huyu aliuawa kwa kupigwa chupa hii,” nikasema.
Polisi wenzangu wote walikubaliana na hilo kwa vile kwenye utosi wa msichana huyo palikuwa na jeraha lililoonesha kupigwa na kitu kizito.
Nikaendelea kuwaeleza polisi wenzangu.
“Kuna chupa nyingine ya bia iko kwenye meza. Inaonesha kuwa huyu msichana alikuwa anakunywa bia na mwenzake.”
“Afande nimefikiria vingine,” polisi mmoja ambaye ananifuatia kwa cheo aliniambia.
“Umefikiria nini?” Nikamuuliza.
“Nimefikiria kwamba mtu aliyemuua huyu msichana anaweza kuwa ni mpenzi wake. Walikuwa wanakunywa halafu ukatokea ugomvi kati yao. Katika ugomvi huo, mtu huyo akampiga chupa msichana huyu kisha akafungua mlango na kukimbia.”
“Fikra yako pia tutaifanyia kazi. Ya kwanza ni ile ya mtu aliyekuwa anamfahamu aliyembishia mlango usiku na alipomfungulia mlango akampiga chupa na kumuua na fikra ya pili ni ya mtu aliyempiga chupa na kumuua alikuwa akinywa naye. Kwa vile tumegundua kuwa mlango umefunguliwa kwa ndani fikira hii ina mashiko.” Nikasema na kuongeza;
“Sasa kitu kingine cha kuchunguza katika tukio hili, ni kutaka kujua aliyemuua huyu msichana ni nani. Kutokana na uchunguzi wetu wa mwanzo tumeshagundua kuwa aliyemuua atakuwa ni mpenzi wake au mtu anayemfahamu au mtu aliyekuwa akinywa naye. Sawa au si sawa?”
“Ni sawa.”
Nikamtazama yule mjumbe ambaye alikuwa amesimama palepale akitusikiliza.
“Tusaidie kitu kimoja. Wewe unafahamu huyu msichana alikuwa akiishi na nani?”
“Alikuwa na mwanaume wake, lakini huyo mtu sijamuona kwa karibu wiki tatu. Inawezekana amesafiri au wameachana,” mjumbe akatueleza.
“Baada ya kutomuona huyo mtu kwa wiki tatu hukuwahi kumuona huyu msichana na mtu mwingine?”
“Siko karibu naye sana kiasi cha kujua maisha yake. Huyo mwanaume wa kwanza nilimgundua kwa sababu alikuwa akiishi naye humu ndani. Ninapofika kwa dharura yoyote ile ninamuona.”
“Wewe kama mjumbe utatusaidiaje. Una hisia juu ya mtu unayemfahamu anayehusika na tukio hili?”
Mjumbe huyo akatikisa kichwa.
“Kwa kweli sina hisia na mtu yeyote.”
Baada ya kujadiliana na polisi wenzangu, polsi mmoja alitoa hoja ambayo haikunipendeza. Alitaka tuwasiliane na kitengo cha polisi cha uchukuaji wa alama za vidole ili kutafuta alama za vidole za mhusika kwenye mlango.
Kitasa nilishakifuta usiku. Kwa hiyo kusingekuwa na alama zozote za vidole labda za mjumbe aliyeingia mle ndani wakati wa asubuhi na kuikuta maiti ile.
Tulikubaliana mtaalam wa kuchukua alama za vidole afike. Baada ya kumpigia simu haikupita hata nusu saa, akawasili kwa gari.
Alipata alama za vidole kwenye mlango upande wa nje na wa ndani wa mlango wa mbele. Alama hizo zinapochukuliwa huwezi kutambua ni za nani mpaka zikafanyiwe uchunguzi. Baada ya alama hizo kufahamika mtu atakayeshukiwa kuhusika na mauaji hayo naye anachukuliwa alama zake za vidole na kulinganisha na zile zilizochukuliwa kwenye kitasa. Kama zitakwenda sawa, muuaji atakuwa ni yeye. Lakini nilishafahamu kuwa katika kitasa hicho cha mlango hapakuwa na alama za muuaji.
Mtaalam wetu wa kuchukua alama za vidole hakutosheka na alama alizoipata kwenye mlango ambazo nilihisi zilikuwa za mjumbe au mtu mwingine aliyeingia humo ndani asubuhi, alichukua pia alama kwenye ile chupa iliyokuwa juu ya meza na kwenye vipande vya ile chupa iliyovunjika. Alituambia kuwa alama zitakazopatikana katika chupa hizo zitakuwa muhimu zaidi.
Ikumbukwe kwamba ile chupa iliyokuwa kwenye meza niliishika mimi wakati ule wa usiku wakati ninakunywa bia. Sasa nikaona balaa linaweza kuniangukia mimi itakapobainika kwamba alama zilizoko katika moja ya chupa hizo ni za kwangu.
Moyo wangu ukaanza kufadhaika hapohapo.
Itaendelea…
Comments